
Wasajili wa Chanjo na Wakurugenzi wanaosimamia uzalishaji wa chanjo za mifugo kutoka nchi 25 za ukanda wa Afrika, wamekutana nchini Tanzania kujadili namna ya kuwa na mfumo wa pamoja wa kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo.
Akifunga mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, amesema mkutano huo umekuja kwa wakati muafaka kwani 16 Juni 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi kampeni ya chanjo za mifugo kitaifa, na ameidhinisha fedha kwa ajili ya kuchanja ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku, sambamba na kuwawekea utambuzi.
"Kikao hiki kina lengo la kuandaa mwongozo ambao utatumika na wazalishaji wa chanjo katika nchi hizo 25, hasa katika kupambana na sotoka ya mbuzi na kondoo. Pia wanakusudia kuanzisha mtandao wa mawasiliano baina yao kwa lengo la kuendelea kupata chanjo bora kwa mifugo ya Afrika" Amesema Prof.Shemdoe.
"Kitu kitakachotengenezwa Tanzania hakitapishana na kile kinachotoka Kenya, Zambia au nchi nyingine yoyote barani Afrika. Ndiyo maana wote wamekusanyika hapa kuridhia mfumo wa pamoja. Chanjo itakayouzwa Tanzania itauzwa sehemu yoyote Afrika bila vikwazo.” Amesema Prof. Shemdoe
Kwa upande wake Mkurugenzi wa AU-PANVAC, Dkt. Bodjo S. Charles, amesema kuwa mkutano huu unalenga kuweka viwango vya pamoja na mwongozo utakaosaidia kufanya ukaguzi na kuthibitisha ubora wa uzalishaji wa chanjo, jambo ambalo litahakikisha kuwa vifaa vyote vya uzalishaji vinazalisha chanjo bora. Baada ya hapo, kutakuwa na mtandao wa wadhibiti wa sekta hii ambao watakuwa wakibadilishana taarifa kati yao.
Kwa upande wake Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Charles Ngassa, amesema kuwa mkutano huu umewakutanisha mamlaka zinazohusika na usajili wa chanjo pamoja na wakurugenzi wanaozalisha vya chanjo barani Afrika, kwa lengo la kupata mwongozo wa usajili wa chanjo ya sotoka ya mbuzi na kondoo.
"Chanjo hiyo ni muhimu sana kwa kutokomeza ugonjwa huo duniani ifikapo mwaka 2030. Kama bara, tunahitaji kuwa na mwongozo mmoja ili kupata chanjo bora kwa mifugo wetu" Amesema DKt. Mayenga
Mkutano huu umeanza tarehe 16 hadi 20 Juni 2025 katika Ukumbi wa King Jada Hotel uliopo Jijini Dar es Salaam.