Back to top

RAIS SAMIA ATAJA MAFANIKIO SEKTA YA NISHATI 2020-2025

28 June 2025
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Sekta ya Nishati imekuwa na mafanikio makubwa  katika kipindi cha miaka mitano. 

Ameyasema hayo wakati akihitimisha shughuli za Bunge Jijini Dodoma,

"Mheshimiwa Spika kutokana na umuhimu wa Sekta ya Nishati kwa maendeleo ya nchi, Serikali imeimarisha upatikanaji wa nishati nchini ikiwemo kukamilisha mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP)”. Amesema Mhe. Samia

Ameongeza kuwa, mbali ya kukamirisha mradi wa Julius Nyerere pia Serikali imekamilisha upelekaji wa umeme katika Vijiji vyote 12,318  nchini.

Ameongeza kuwa, msukumo uliofanywa na Serikali katika sekta ya nishati umewezesha uzalishaji wa umeme kuongezeka hadi kufikia megawati 4031.71 kutoka megawati 1,601.84 mwaka 2020.

"Hali hii imechangiwa na miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme ukiwemo mradi wa kielelezo wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere wenye megawati 2115, vilevile mradi wa Kinyerezi I Extension wa megawati 185 na mradi wa Rusumo ambao tumeutekeleza kwa ushirikiano wa Nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda kwa mgawanyo wa megawati 26.67 kwa kila Nchi”. Amesema Rais Samia

Katika miradi ya usafirishaji umeme amesema Serikali imekamilisha miradi ya usafirishaji umeme ya kutoka Singida hadi Arusha, Geita hadi Nyakanazi, na Julius Nyerere hadi Chalinze.

Miradi mingine ni Nyakanazi hadi Kigoma, Tabora hadi Urambo, Rusumo hadi Nyakanazi na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenye njia ya Reli.

Amesema mafanikio hayo yameongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha ameeleza kuwa,  Serikali imefanikiwa kuiunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi na gridi ya Taifa.

Kuhusu umeme Vijijini, Rais Samia amesema Tanzania imefikia hatua kubwa na ya kihistoria kwa kuunganisha Vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara na huduma ya umeme.

Amesisitiza kuwa, kwa sasa Serikali inapeleka umeme kwenye Vitongoji ambapo vitongoji 33,657 tayari vimeshafikishiwa umeme kati ya Vitongoji 64,359 sawa na asilimia 52.3.

Kuhusu nishati mbadala, amesema Serikali inampango wa kuzalisha nishati mbadala kwa kutumia vyanzo jadidifu ambapo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuanza kufikiria kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya Nyukilia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema  Serikali inapanga kuweka ushindani katika Sekta ya nishati kwa kuialika sekta binafsi kushiriki kuongeza upatikanaji wa umeme.