Back to top

ATAKAYEBAINIKA KWA WIZI KUCHUKULIWA HATUA

12 September 2025
Share

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuhusika na wizi au uharibifu wa miundombinu ya umeme, kwani vitendo hivyo ni uhujumu uchumi vinavyosababisha hasara kubwa kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa Septemba 11, 2025 na Afisa Usalama Mwandamizi wa TANESCO, Bw. Steven Maganga, katika zoezi la ukaguzi wa mita lililofanyika Magomeni, Mburahati jijini Dar es Salaam.

Katika ukaguzi huo, TANESCO ilibaini baadhi ya wateja kufungua mita na kuweka vifaa maalumu (Resistor) vinavyopunguza kasi ya usomaji wa matumizi halisi ya umeme.

“Tumembaini mteja ambaye ameharibu miundombinu kwa makusudi kwa kufungua mita na kuweka Resistor ili kupunguza usomaji wa matumizi tofauti na hali halisi,” alisema Bw. Maganga.

Aidha, katika eneo la Tandale Shirika limegundua mteja mmoja kuhamisha mita iliyosajiliwa Manzese na kuipeleka Tandale kinyume cha sheria. TANESCO imesitisha huduma ya umeme katika nyumba hiyo na kumtaka mteja husika kulipa gharama zote stahiki.

Kwa upande wake, mmoja wa wateja aliyehusishwa na tukio la kuhamisha mita aliomba Shirika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu sahihi za kuhamisha mita, akiahidi kulipa gharama zote zinazostahili.

TANESCO inasisitiza kuwa itaendelea na ukaguzi wa mita nchi nzima na kuwataka wananchi kufuata utaratibu sahihi wa kuunganishiwa au kuhamishiwa mita. Imewatahadharisha wote watakaohusika na hujuma kuwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo mashitaka ya uhujumu uchumi, malipo ya gharama na adhabu za kifungo.