
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Manispaa ya Tabora imenufaika kwa kiwango kikubwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya serikali ya awamu ya sita.
Amesema kukamilika kwa Hospitali ya Manispaa ya Tabora na majengo ya huduma za afya kumeimarisha upatikanaji wa matibabu, huku sekta ya elimu ikipiga hatua kwa ongezeko la shule za msingi kutoka 819 mwaka 2020 hadi 960 mwaka 2025 na sekondari kutoka 197 hadi 277.
Dkt. Samia amesema huduma ya maji safi pia imeimarishwa, sambamba na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima, usambazaji wa dawa za ruzuku na chanjo kwa mifugo. Aidha, amesema miradi ya ujenzi wa soko kuu na stendi, ukarabati wa Kiwanja cha Ndege Tabora na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) vinadhihirisha dhamira ya serikali kuifanya Tabora kitovu cha maendeleo.
Akizungumzia ahadi kwa miaka mitano ijayo, Dkt. Samia amesema serikali yake itajenga shule mpya nne, mabweni 16, nyumba 46 za walimu, vyumba 19 vya TEHAMA, maktaba 17 na majengo ya utawala 12 katika sekondari za Manispaa hiyo. Ameongeza kuwa serikali itakamilisha mradi wa mtandao wa maji safi na taka, barabara ya Tabora–Ipole–Koga–Mpanda (km 202), na kujenga minada mitatu ya mifugo, majosho matano, malambo 20 pamoja na mabwawa ya samaki 20 na soko la samaki moja.