Back to top

MAAFISA RASILIMALIWATU RUKWA WAASWA KUTIMIZA WAJIBU WAO.

18 September 2025
Share

Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu kutoka Halmashauri za wilaya mkoani Rukwa wameaswa kutimiza wajibu wao ili watumishi waweze kupata haki zao wanazostahili kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Kaimu Afisa Mfawidhi PSSSF mkoa wa Rukwa Bw. Paul Mbijima, wakati akifungua kikao kazi baina ya Mfuko na Maafisa hao mjini Sumbawanga.


Alisema Maafisa Rasilimaliwatu wanapaswa kuwahimiza watumishi wanapoajiriwa kuhakikisha taarifa zao zinakuwa sahihi.


“ Ninyi kama kiungo baina ya Mfuko na watumishi, mkitimiza wajibu wenu mtawasaidia watumishi kupata haki zao kwa wakati,” alisema Bw. Mbijima
Alitoa mfano wa baadhi ya mafao ya muda mfupi ambayo yana ukomo wa kuyaomba kama vile fao la uzazi na fao la msaada wa mazishi.


“ Fao la uzazi linapaswa kuombwa ndani ya siku 90 sawa na miezi mitatu, na fao la msaada wa mazishi linapawswa kuombwa ndani ya siku 30 sawa na mwezi mmoja, mafao hayo mawili yakiombwa nje ya muda huo yanakataliwa na mfumo na hivyo mtumishi anakuwa amekosa haki zake.” Alifafanua.


Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho wamesema, elimu waliyoipata imewasaidia kuwakumbusha wajibu wao.


“Mtumishi anapoajiriwa kwa mara ya kwanza ndio maandalizi yake ya kustaafu yanapoanza, hivyo taarifa zake zinapaswa kuwa sahihi na sisi ndio tunaowajibika kuhakikisha hilo.” Alisema Bw. Hamisi Himidi, Afisa Rasilimaliwatu Hospitali ya Rufaa mkoa wa Rukwa.


Naye Afisa Utumishi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Bw. Mankron Seneda, yeye amesema utaratibu mpya wa usajili wa watumishi kwenye mfumo utaondoa malalamiko yaliyokuwepo kwa watumishi wanapofikia muda wa kustaafu ambapo moja ya nyaraka ni kuwasilisha barua ya kuajiriwa.


“ Tumeelezwa kuwa mtumishi mpya anayeajiriwa wakati wa usajili, moja ya nyaraka ni kuambatisha barua ya ajira, hii itaondoa usumbufu atakapofikia muda wa kustaafu kwani tayari nyaraka hiyo itakuwa kwenye mfumo na hapatakuwa na usumbufu wa kuitafuta.” Alisema.