
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amewataka Mawakili wa Serikali kuyatumia mafunzo yanayotolewa kuhusu Hifadhi ya Jamii, katika kuhakikisha kuwa Sheria na Kanuni za Hifadhi ya Jamii zinalinda na kusimamia haki na maslahi ya Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu Hifadhi ya Jamii kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika Chuo cha Uongozi Mwalimu Nyerere, Kibaha, Mkoani Pwani.
Alisema kwa kushiriki mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watanufaika kwa kuongeza ujuzi kwenye masuala mbalimbali husasan sheria zinazohusiana na Hifadhi ya Jamii ikiwemo , Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma [Sura ya 371], Sheria ya Mikataba [Sura ya 345], Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini [Sura ya 366], pamoja na Usimamizi wa Fedha na Uwekezaji.
“Ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yatajikita katika maeneo Muhimu ya Kisheria na Kiutawala ikiwemo Muundo wa kisheria wa PSSSF na majukumu yake ya msingi, Haki na Wajibu wa wanachama, wastaafu na wategemezi wao.” Amesema Mhe. Johari.
Aidha, kupitia mafunzo hayo Mawakili wa Serikali wataweza kuwa na uelewa mpana wa kushauri na kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu Mfuko wa PSSSF, kupunguza migogoro inayoweza kupelekea kesi Mahakamani kwa kutumia mbinu za Usuluhishi na mazungumzo na kuweka misingi thabiti ya kisheria katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za Mfuko na kujenga uhusiano wa karibu kati ya PSSSF na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa manufaa ya Taifa, amesema.
Mhe. Johari alitoa wito kwa Mawakili wa Serikali wanaoshiriki mafunzo hayo kuwa na ari na kuhakikisha kuwa maarifa watakayoyapata wanayaweka katika Vitendo na kuhakikisha kuwa PSSSF inaendeshwa kwa ufanisi na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni.
“ Wajibu wetu ni kuhakikisha kuwa PSSSF inaendeshwa kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria na kanuni, na hivyo kulinda haki za wanachama wake.” Alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF na Uongozi kwa kuandaa na kufadhili mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali kwakuwa yatawasaidia kupata uelewa wa kitaalamu na kisheria ili kuongeza weledi katika sheria, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za Hifadhi ya Jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF Bi. Vupe Ligate amesema kuwa wanaendesha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kwa lengo la kuwaongezea uelewa juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Hifadhi ya Jamii ambayo yatawarahisishia utendaji kazi wao wakati wakitoa ushauri wa Kisheria kuhusiana na Hifadhi ya Jamii.