
Mgombea ubunge kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Jimbo la Nanyumbu, Hamad Hasheem ametangaza kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), huku akisema amevutiwa na mienendo na utekelezaji wa ajenda za Chama hicho baada ya kuangalia mikutano ya mgombea urais wa chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kugundua kuwa ni mtekelezaji wa yale anayoahidi.
Amesema hayo leo Septemba 23, 2025 kwenye kampeni za mgombea urais wa CCM, Samia akiwa Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
"Ndugu zangu ninasema Samia anaweza, nimepata majibu leo, nimepata majibu Kigoma nilikuwa nafuatilia kampeni za mama Samia, Nimeridhika kwa moyo wa dhati," amesema.
"Nilifikiri miradi mikubwa aliyoacha Hayati John Magufuli, mradi wa Busisi mama kapita nao, ameleta vichwa vya treni vya kisasa. Daraja la Busisi limenifanya niamini kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki sidhani kama ana mwenzake. Leo ninatangaza nakihama Chama cha ACT Wazalendo, navaa jezi ya kijani na njano naombeni mnikaribishe,"