
Viongozi Wakuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Ndg. John Heche, wameburuzwa mahakamani baada ya kukiuka amri ya Mahakama Kuu iliyoweka zuio la shughuli za kisiasa kwa chama hicho.
Kwa mujibu wa shauri jipya lililofunguliwa katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, imeelezwa kuwa viongozi hao wameonyesha kupuuza amri ya mahakama zaidi ya mara moja.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo iliyotolewa na Wakili wa walalamikiwa Mulamuzi Byabusha, licha ya zuio hilo kati ya mwezi Juni hadi Septemba, Bw. Heche na wenzake walionyesha kukaidi amri hiyo ya Mahakama. Imeelezwa kuwa katika kipindi hicho wadaiwa waliendelea kuitisha na kuandaa mikutano mbalimbali.
Kulingana na hati hiyo ya kiapo kina Heche wanadaiwa kufanya mikutano ya ndani ikiwemo Ile ya Wandishi wa habari na kutoa maelekezo kadhaa ya kisiasa. Hali inayoonyesha kukaidi na kupuuza Amri Halali ya mahakama hiyo.
Ikumbukwe zuio hilo la mahakama lilitolewa na Mahakama Kuu Juni 10, 2025 kufuatia shauri namba 8960 la mwaka 2025. Shauri linalohusu mgawanyo wa Mali za CHADEMA kati ya Bara na visiwani lilifunguliwa na Bw. Mohamed na wenzake.
Kwa mujibu wa shauri jipya linalomkabili Heche na wenzake, imeelezwa kuwa mbali na amri ya mahakama wadaiwa hao wameonekana kupuuza na kutozingatia.
Imeelezwa kuwa katika kipindi hicho cha mwezi Juni hadi Septemba Heche, Mnyika na wenzao waliendelea kufanya mikutano na kuhamasisha mambo mbalimbali ya kisiasa kinyume na Amri ya mahakama hiyo.
Mbali na Heche na Mnyika, viongozi wengine wanaokabiliwa na tuhuma hizo ni Rose Mayemba na Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya na Gervas Bernard Lyenda.