
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), imeendelea kusogeza huduma karibu na wateja wake kwa kuwatembelea wauzaji wa bidhaa zake katika mikoa ya Iringa na Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika kitaifa kuanzia Oktoba 6 hadi 11, 2025.
Ziara hizo zilifanyika tarehe 9 na 10 Oktoba 2025, zikiongozwa na Afisa Masoko wa TVLA, Bw. Fihiri Mbawala, ambaye alitembelea maduka mbalimbali yanayouza bidhaa za TVLA, hususani chanjo za mifugo, kwa lengo la kusikiliza maoni ya wateja, kupokea changamoto na kujadiliana kuhusu maboresho ya huduma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Mbawala alisema TVLA imeamua kutumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kama jukwaa la kujenga uhusiano wa karibu zaidi na wadau wake wa sekta ya mifugo.
"Tunatambua kwamba mafanikio ya TVLA yanategemea kuridhika kwa wateja wetu, ndiyo maana tumeamua kutoka ofisini na kuwatembelea moja kwa moja, ili kusikia kutoka kwao nini kifanyike kuboresha huduma" Amesema Bw. Mbawala.
Ameongeza kuwa TVLA itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora, salama na zenye ubora wa kitaifa na kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa mawasiliano endelevu kati ya wauzaji na taasisi hiyo.
Kwa upande wake Bi. Zainabu Mdegela muuzaji wa bidhaa za TVLA kutoka mkoani Iringa alisema kuwa TVLA imeonyesha dhamira ya dhati katika kuwajali wateja na ameshukuru kuona viongozi wa TVLA wanawafikia moja kwa moja madukani kitu kinachowapa nafasi ya kueleza changamoto wanazokutana nazo na kutoa ushauri wa kuboresha huduma.”
Naye Bw. John Mushi kutoka Dodoma ameshauri kuimarishwa kwa mawasiliano ya taarifa za bidhaa na bei kupitia njia za kidijitali, sambamba na kutoa mafunzo zaidi kuhusu utunzaji wa chanjo.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka duniani kote kwa lengo la kutambua mchango wa wateja na kuhimiza taasisi mbalimbali kuboresha ubora wa huduma. TVLA imekuwa miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotumia wiki hiyo kujenga ushirikiano na wadau wake wa sekta ya mifugo.