Back to top

SERIKALI IMETOA BIL 424.6 UTEKELEZAJI MIRADI YA TANROADS RUKWA

20 October 2025
Share

Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 424.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Kitaifa, ikiwemo Ukarabati wa Uwanja wa Ndege Sumbawanga na ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami, na kazi za matengenezo ya barabara pamoja na kazi za dharura zilizotekelezwa zikijumuisha miradi ya usanifu wa Barabara za TANROADS mkoa wa Rukwa.

Mkoa wa Rukwa una mtandao wa Barabara wa Kilometa 1250.84, katika mtandao huo, Barabara kuu ni kilometa 415.86 na Barabara za mkoa ni kilometa 834.98 kati hizo barabara kuu za lami ni Kilometa 298.35 na Barabara kuu changarawe ni kilometa 117.51. Kwa upande wa Barabara za Mkoa kiwango cha lami ni kilometa 76.83 na Barabara za mkoa Changarawe ni Kilometa 758.15.

Akizungumza mjini Sumbawanga Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga, amesema kuwa serikali inaendelea na ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga ambao umefikia asilimia 86 na unajengwa na Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Co Ltd, chini ya Mhandisi Mshauri SMEC International kwa ushirikiano na SMEC Tanzania Ltd chini ya ufadili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kwa gharama ya shilingi Bilioni 60.1

Mhandisi Mwanga amesema kuwa serikali inaendelea na kazi ya dharura ya ujenzi wa madaraja 3 katika Barabara ya Kasansa – Kilyamatundu yaliyoharibika kutokana na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya kwa gharama ya shilingi Bilioni 23.183 yanayojengwa na Mkandarasi M/s STECOL Corporation huku Mhandisi Mshauri akiwa ni TECU. Miradi hiyo ni Pamoja na ujenzi wa daraja la Kisa lenye urefu wa meta 40, Kinambo II lenye urefu wa meta 50 na Daraja la Ilemba (Mkanga I&II) lenye urefu wa meta 60. Miradi yote hii inafadhiliwa na Benki ya Dunia. “Daraja la 4 ni la Lwanji lenye urefu wa meta 200 ambalo lipo katika hatua za manunuzi lililopo katika mji mdogo wa mto Wisa kwa gharama ya shilingi Bilioni 28” Amesisitiza

Ameutaja mradi uliokamilika kuwa ni Mradi wa Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami ya Sumbawanga – Matai – Kasanga ulifadhilia na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 yenye urefu wa kilometa 107 uliyogharimu shilingi bilioni 133.286 kupitia mkandarasi CR15 kwa ushirikiano na New Century zote za nchini China.

Mhandisi Mwanga ameutaja mradi mwingine wa kimkakati unaoendelea ambao ni Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami ya Ntendo – Muze – Kilyamatundu iliyofadhiliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 yenye urefu wa kilometa 179 ambapo utekelezaji kwa awamu ya kwanza umeanza na kilometa 25 kutoka Ntendo – Kizungu unaotekelezwa na mkandarasi CGC huku ukisimamia wa mhandisi mshauri ni 7 Engeneering Co Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 45.299

Amesema kuwa kukamilika kwa uwanja wa ndege Sumbawanga, Barabara na madaraja kutarahisisha huduma za biashara, kupunguza muda wa usafiri na usafirishaji, urahisi wa wananchi kufikia huduma za jamii Pamoja na kuipunguzia serikali gharama za mara kwa mara za matengezo ya Barabara na kutafungua fursa za kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hususani kulifikia soko la SADC kiurahisi na lango kuu la kuingilia nchi za SADC.