
Siku chache baada ya uzinduzi rasmi wa programu maalum ya Konekt Umeme, Pika kwa Umeme uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanza kutekeleza kwa mafanikio makubwa zoezi la kuwaunganishia wananchi umeme pamoja na kuwapatia kwa mkopo majiko ya umeme kwa ajili ya kupikia.
Programu hii, inayotekelezwa nchi nzima, ni sehemu ya Mpango wa Kitaifa wa Nishati (Energy Compact) unaolenga kuwaunganishia umeme wananchi milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030, sawa na takribani wateja wapya milioni 1.7 kila mwaka.
Wananchi katika mikoa mbalimbali wameanza kunufaika na mpango huu tangu kuanza rasmi kwa zoezi hilo. Wengi wameeleza kufurahishwa na mpango huo, hususan kwa kuwa unalenga kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata majiko ya umeme kwa utaratibu wa mkopo, hali iliyowasaidia kuanza kutumia nishati safi na salama kwa kupikia.
Aidha, wananchi hao wameiomba TANESCO kuhakikisha majiko yanayotumia umeme kwa kiwango kidogo yanapatikana kwa wingi kutokana na mahitaji makubwa yaliyojitokeza.
Wameeleza kuwa matumizi ya umeme kwa kupikia ni nafuu na salama zaidi ikilinganishwa na nishati nyingine kama mkaa na kuni, hivyo ni muhimu elimu ya matumizi ya umeme jikoni ikaendelea kutolewa kwa wananchi.
Utekelezaji wa mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mradi wa Modern Energy Cooking Services (MECS) chini ya Serikali ya Uingereza, ambapo wateja wapya waliounganishiwa umeme wataweza kulipia majiko hayo kwa awamu kupitia manunuzi yao ya umeme.