
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayogusa moja kwa moja ustawi wa wananchi.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi ya mazungumzo na viongozi wa bodi na menejimenti za taasisi hizo, Mhe. Ndejembi alisisitiza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kupaumbele kwa Taifa kwani Serikali inategemea utendaji wa weledi, uwajibikaji na uwazi kutoka kwa taasisi hizo ili kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa.
“Napenda kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa nafasi hii, nimeona ni vyema kukutana nanyi kwa lengo la kufahamiana, kujifunza lakini pia kuhakikisha tunaweka sawa mikakati mathubuti katika utekelezaji wa majukumu yetu lakini pia kuhakikisha tunaongeza kasi na bidii katika kutekeleza majukumu yetu ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini”. Amesisitiza Mhe. Ndejembi.
Waziri Ndejembi pia amewataka viongozi wa TPDC na PURA kuhakikisha wanazipitia changamoto zinazoathiri kasi ya utekelezaji wa miradi na kuwasilisha mapendekezo ya maboresho yatakayowezesha kuongeza tija huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika kipindi hiki ambapo Serikali imewekeza nguvu kubwa katika kukuza miundombinu ya nishati na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, aliwahimiza viongozi kuendelea kujenga utamaduni wa kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti mbalimbali hasa katika mafuta na gesi kwani sekta ya mafuta na gesi ina ushindani mkubwa duniani na hivyo inahitaji uongozi thabiti, mipango madhubuti na matumizi bora ya rasilimali ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na rasilimali zake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Petroli Tanzania Mussa Makame amemshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kuboresha mifumo ya utendaji pamoja na kuimarisha ushirikiano wa taasisi kwa maslahi mapana ya Taifa huku akiahidi kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha malengo ya taifa yanafikiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni ameeleza namna taasisi hiyo ilivyojikita Katika kuanzisha vyanzo vya mapato huku akiahidi kutekeleza yote yaliyoagizwa pamoja na kuongeza uwazi katika usimamizi wa miradi kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za maendeleo ya miradi ya nishati inayotekelezwa nchini.
