
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za wizi wa mita za maji katika maeneo ya Area Six, Kichangani, na Tubuyu.
Miongoni mwa mita zilizoibwa ni pamoja na zile zilizokuwa katika makazi ya Abdallah Mohammed wa mtaa wa Tubuyu Tungi, Kirian Jonas wa Nane Nane, Prisca Albert Kobero, na Leah Jackson ambao ni wakazi wa Kichangani.
Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni Christopher Peter (19), Draston James (16), Yohana Wiliam (17), Nestory Antony (17), na Antony Godfrey (17), wote wakiwa ni wakazi wa mtaa wa Area Six, Kata ya Kichangani.
Jeshi hilo limeeleza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani punde upelelezi utakapokamilika ili kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kufuatia kukamatwa kwa vijana hao, Jeshi la Polisi mkoani humo limetoa wito kwa wananchi, hususan vijana, kuachana na vitendo vya uhalifu na badala yake wajishughulishe na kazi halali za kuwaingizia kipato.
Vilevile, polisi imewasihi wazazi na walezi kuendelea kusimamia malezi bora na kudumisha maadili mema kwa watoto wao ili kuepusha vitendo vya uhalifu katika jamii.
