
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wanaoshiriki Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali walipe kipaumbele zaidi suala la kutafuta ufumbuzi wa nishati safi ya kupikia na hasa katika kipindi hiki cha mpito.
Ametoa wito huo Oktoba 29, 2026 wakati akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kikao kilichofanyika Ikulu ya Kremlin, jijini Moscow, Urusi.
Waziri Mkuu amewaeleza wakuu wa nchi waliohudhuria mkutano huo kwamba suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele muhimu kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan amejitolea kutetea jambo hilo katika bara lote la Afrika.
Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi hao kuhusu Azimio la Nishati la Dar es Salaam la mwaka 2025 ambalo lilikuja na mpango kabambe unaolenga kutoa umeme wa kuaminika kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030.

"Ili kufikia malengo haya ya kikanda, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakaribisha kwa dhati ushirikiano wa kimkakati katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, ikitumia utaalam wa Urusi unaotambulika duniani kote katika teknolojia ya hali ya juu ya nishati"
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema kuwa kila mshirika wa kimataifa, ikiwemo Shirikisho la Urusi, wanapaswa kushirikiana na Afrika katika kuendeleza uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi na kuongeza thamani ya malighafi katika bara la Afrika.
Amesema kuwa, ushirkiano huo hasa katika madini ya mkakati, lazima uelekezwe katika kuanzisha viwanda vya uchakataji ndani ya bara la Afrika, kuhamisha teknolojia za kisasa na kutengeneza ajira endelevu, ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi barani Afrika
"Bara linalouza madini ghafi kisha kununua tena betri zilizotengenezwa kutokana na madini hayo litaendelea kuwa maskini, bila kujali idadi ya mikutano ya kilele litakayohudhuria".
