
Serikali imesema hakuna tatizo la mzunguko wa fedha kuwa mdogo nchini kwani imechukua hatua mbalimbali katika utekelezaji wa sera ya fedha ambayo imesaidia kuimarisha hali ya ukwasi kwenye benki za biashara.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Ashatu Kijaji ameliambia bunge hatua zilizochukuliwa na serikali ni pamoja na kushusha kiwango cha riba katika soko la fedha baina ya mabenki.
Amesema kiwango cha riba kimeshuka kutoka asilimia ishirini na moja mwaka 2016 hadi asilimia kumi na saba mwaka 2018 huku mikopo ya sekta binafsi ikiongezeka kutoa asilimia 1.7 hadi kufikia asilimia 7.3.
Dkt.Kijaji amesema Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi, ili kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko.
Aidha, amesema hatua zingine ni pamoja na kushusha riba kutoka Benki Kuu kutoka asilimia kumi na sita hadi asilimia saba na kupunguza kiwango cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara kutoka asilimia kumi hadi asilimia saba.