
Rais wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amemuapisha Balozi Batilda Salha Burian kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Rais Samia pia amemuapisha Zuwena Omary Jiri kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza baada ya viongozi hao kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Ametaka wasimamie huduma zinazotolewa na watumishi wao ili huduma hizo ziwe na ubora unaotegemewa na wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Ummy Mwalimu amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Batilda Salha Burian kusimamia mapato katika Mkoa wake kwa sababu kuna baadhi ya wilaya katika mkoa huo hazifanyi vizuri katika ukusanyaji wa mapato.