Back to top

WAZIRI ANGELLAH KAIRUKI MGENI RASMI KCF.

26 December 2023
Share

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye Tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival (KCF), litakalofanyika Desemba 27 na 28 viwanja vya Kilihome Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Mwenyekiti wa Kilimanjaro Cultural Festival (KCF) Ansi Mmasi, amesema Mhe Kairuki atakuwepo Kilihome tararehe 28, ambapo pamoja na mambo mengine atazindua program maalum ya homestay inayotoa fursa kwa wananchi wa Kilimanjaro kujisajili na kuruhusu nyumba zao zitumike kwa malazi ya wageni watakaofika kwa shughuli mbalimbali za utalii na kutembelea vivutio vilivyopo Mkoani Kilimanjaro.

Pia Waziri Kairuki atakabidhi zawadi kwa vikundi vya washindi wa ngoma za asili na watoto wa umri wa Kati ya miaka 19 hadi 18  waliofanya vizuri kwenye shindano la kuzungumzia vivutio vya asili katika maeneo yao kwa lugha fasaha za asili za makabila yao.

Mmasi akasema siku ya kwanza ya tamasha litakalofunguliwa Rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, timu ya msafara wake itatembelea mapango ya asili ya Chagga curve yaliyopo Marangu na msafara mwingi utaelekea Kibosho Kirima kutembelea mapango ya asili ya Nubi curve.

Akabainisha licha ya mkoa kuwa na vivutio vingi, sio rahisi kwa siku moja kuvimaliza vyote, kwahiyo hatua hiyo ni sehemu ya kufungua njia kwa wanakilimanjaro na watanzania wote, na hata wageni kutembelea vivutio mbalimbali vikiwemo vya asili vilivyopo maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro.

Akawasihi Wana Kilimanjaro kutumia tamasha hili kujifunza, kushauri na kuboresha zaidi ili matamasha mengine ya aina hii yaendelee kuleta tija kwa wana jamii wa Kilimanjaro.

"Fikeni kujionea Ngoma za asili, vyakula na vinywaji vya asili kama Kirembwe, ugali wa ndizi, Ikatwe, ngararimu, ndizi choma za magadi, mbege, dengerua,kitalolo cha maziwa,kitawa,kiburu nk, wale, wanywe, lakini waone Ngoma za makabila ya asili ya wachaga, wapare na wamasai na mambo mengi mazuri"Alisema Mwenyekiti huyo wa KCF.

Mmasi akasema maandalizi ya tamasha hilo tayari yamekamilika, na hakuna kiingilio chochote hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi Kilihome kushuhudia mambo mengi mazuri yatakayoimarisha na kuelimisha kuhusu Mila, tamaduni na desturi pamoja na kufahamu vivutio vya asili vilivyopo Kilimanjaro.

KCF ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa kupitia mawazo ya kundi sogozi la WhatsApp la wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wanaoishi ndani na nje ya mkoa huo, baada ya kukutana ana kwa ana 2019 na kushauriana kutumia nafasi hiyo kuwa na kitu chenye mlengo chanya wa maendeleo ya kusaidia jamii ya wanakilimanjaro na Taifa kwa ujumla.