
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imejipanga kuimarisha upatikanaji wa nishati, kuwawezesha wanawake kupitia nishati safi ya kupikia, na kuongeza fursa za vijana kwa mafunzo ya ufundi stadi.
Akizungumza leo, Septemba 3, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Vwawa mkoani Songwe, Dkt. Samia amesema hatua kubwa zimefikiwa katika sekta ya umeme, lakini bado kuna kazi ya kuimarisha usambazaji wake ili kufikia viwango vinavyohitajika.
“Kazi imefanyika, umeme sasa sio shida sana, lakini bado kuna kazi inahitajika. Tumejipanga kujenga njia ya kusafirishia umeme kutoka Iringa kwenda Songwe ya kilovoti 730, ambapo 400 zitatumika kwenye mikoa yetu na 330 tutauza Zambia kwa majirani zetu,” amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia amesisitiza dhamira ya serikali kuendeleza kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan kwa wanawake. Amesema upatikanaji wa vituo vya kubadilishia mitungi ya gesi ni kipaumbele, na serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote.
“Wanawake wa Tanzania wameipokea kampeni ya nishati safi na wanaifanyia kazi kweli kweli. Tunawaahidi kwa yale maeneo ambayo vituo vya kubadilisha mitungi havipo, tutahamasisha sekta binafsi wasogee huko, kwa sababu tayari tumewatengenezea soko,” amesema.
Kwa upande wa vijana, Dkt. Samia amesema serikali itaendelea kuwawezesha kupata ujuzi kupitia vyuo vya VETA, ambapo gharama za masomo zitalipwa na serikali.
“Vijana wakimaliza VETA wanapata ujuzi wa moja kwa moja. Malipo ni kwa serikali, vijana hawalipi. Kama tunavyolipia shule ya msingi hadi sekondari, ndivyo tunavyowalipia pia VETA, na wanaingia kwenye mpango wa mikopo ya wanafunzi,” amesema.