
Rapa Jay-Z amejumuishwa kwenye tuhuma za kumbaka na kumnyanyasa kingono msichana wa miaka 13 kwenye sherehe iliyoandaliwa na Sean “Diddy” Combs mwaka 2000, kulingana na kesi iliyofanyiwa marekebisho na kuwasilishwa katika Mahakama ya Shirikisho siku ya Jumapili.
Mwanamke anayedai kuwa alinyanyaswa kingono na Sean “Diddy” Combs amerekebisha madai ya kesi yake na kumjumuisha pia Shawn Carter maarufu kama Jay-Z kwenye tukio la sherehe hiyo.
Kesi hiyo hapo awali iliwasilishwa dhidi ya Combs mnamo Oktoba, lakini Jumapili mwanamke huyo aliongeza Shawn Carter, rapper na mfanyabiashara anayejulikana kama Jay-Z, kama mshtakiwa katika kesi ya madai.
Carter ndiye mtu mashuhuri wa kwanza kushtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia kushirikiana na Combs.
Kesi hiyo iliyorekebishwa, iliyowasilishwa Jumapili katika Wilaya ya Kusini ya New York, inadai kwamba msichana huyo alipewa dawa za kulevya na kubakwa wakati wa tafrija iliyoandaliwa na Combs kufuatia Tuzo za Muziki za MTV huko New York. Malalamiko ya awali, yaliyowasilishwa mwezi Oktoba, yalimtaja Jay-Z kama "Mtu Mashuhuri A" lakini haikumtaja kama mshtakiwa.
Jay-Z amekanusha madai hayo, akitaja kesi hiyo kama "jaribio la uwongo" lililoratibiwa na timu ya wanasheria wa mlalamikaji.