Back to top

"NDEGE YETU HAIJATELEKEZWA MALAYSIA" - ATCL

12 May 2024
Share

Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imekanusha taarifa za ndege yake aina ya Boeing 787-8, yenye usajili namba 5H-TCJ, kupelekwa kwenye matengenezo makubwa (Check - C), kabla ya kufikisha muda wake tangu inunuliwe na kutelekezwa nchini Malaysia, ambapo limeeleza kuwa ndege hiyo imepelekwa nchini Malaysia kwa ajili ya matengenezo ya lazima ya injini zake baada ya kufikisha muda wake na sio matengenezo makubwa ya Check - C.

ATCL imesema matengenezo makubwa ya ndege zake 787-8 (Dreamliner) hufanyika hapa nchini kwenye karakana yake ya KIMAFA iliyopo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, kila baada ya miaka 3 au masaa 12,000, kwani karakana hiyo ina wataalamu wenye uzoefu wa kufanya matengenezo makubwa ya ndege ya kiwango cha Check - C.
.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa chanzo cha ndege hiyo kukaa muda mrefu kwenye karakana, Malaysia, inatokana na uhaba wa injini za ziada ambazo zingeweza kutumika wakati injini za ndege hiyo zikifanyiwa matengenezo, na kwamba injini hizo zinapopelekwa kwenye matengenezo hayo zinalazimika kukaaa kwenye foleni kutokana na idadi kubwa ya injini zinazosubiria matengenezo.

Hata hivyo ATCL imesema, matengenezo hayo yanaendelea na ndege hiyo inatarajiwa kurejea nchini mwanzoni mwa mwezi Juni 2024.