Back to top

TAWIRI YAZINDUA CHUMBA CHA KUHIFADHI SAMPULI ZA VIUMBE HAI

13 December 2024
Share

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), kwa kushirikiana na Taasisi ya Bioanuai ya Korea Kusini (NIBR), imezindua chumba maalum cha kuhifadhi na maonesho ya viumbe hai ambao ni wadudu, Mimea na Wanyama, ambacho kitatumika kwa ajili ya utafiti na kutoa elimu kwa umma kuhusu bioanuai nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mgeni Rasmi  ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Alexander Lobora, ameipongeza Jamhuri ya Korea kupitia (NIBR) kuwezesha ujenzi wa chumba hicho maalum chenye tija katika uhifadhi na elimu ya bioanuai.

“Nitoe wito kwa TAWIRI kukusanya sampuli za kutosha ili kuwezesha na kuongeza tafiti za bioanuai, kuongeza hamasa ya kutunza bioanuai kupitia mafunzo na maonesho "amehimiza Dkt. Lobora.

Mkurugenzi wa Utafiti TAWIRI Dkt. Julius Keyyu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu TAWIRI amesema chumba cha kuhifadhia Bioanuai kitasaidia watafiti hususan wanafunzi wasio na bajeti ya kutosha kufanya tafiti kwa urahisi kwa kutumia sampuli zilizokusanywa,  kutoa elimu ya Bioanuai pamoja na maonesho.

“Chumba hiki ni cha kipekee hapa nchini, na cha viwango vya kimataifa kwa kuwa kinadhibiti wadudu waharibifu, kina miundombinu ya kudhibiti joto na unyevunyevu ili kuhifadhi sampuli za wadudu, wanyama, na mimea  kwa muda mrefu na vizazi vijavyo”ameeleza Dkt. Keyyu

Naye, Mkurugenzi wa Utafiti wa Bioanuai kutoka Taasisi ya kuhifadhi Bioanuai ya Korea Kusini (NIBR) Dkt. Jae - shin Kang amesema Nchi hiyo imekuwa na Ushirikiano na Tanzania kwenye Tafiti za Bioanuai toka mwaka 2014 ambapo katika kuimarisha uhifadhi wa bioanuai wametoa mafunzo ya kukusanya, kuandaa na kuhifadhi sampuli za bioanuai  kwa watafiti kumi na mbili (12) kutoka TAWIRI.

“Kumekuwa na machapisho mengi  ya bioanuai ila bado  kuna umuhimu wa kuwa na vitu vinavyoonekana kwa uhalisia” .

Hafla hiyo ya Uzinduzi imefanyika Makao Makuu ya TAWIRI -Njiro Arusha na kuhudhuriwa na watafiti kutoka TAWIRI, NIBR -Korea Kusini ,taasisi za TANAPA, NCAA, TAWA, TPHPA, Taasisi ya Kiafrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) na Kituo cha Makumbusho ya elimu Viumbe cha Arusha.