Naibu Waziri wa Afya, Dkt.Godwin Mollel, amewataka wataalamu wa tiba asili nchini, kuachana na matumizi ya viungo vya binadamu na wanyama katika huduma zao, na kwamba dhana potofu zinazohusisha ngozi ya nyati, simba, na mkia wa nyumbu zinapaswa kukemewa kwa nguvu zote.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili, Kitaifa yaliyofanyika Jijini Mwanza, yaliyoratibiwa na Wizara ya afya chini ya baraza la tiba asili na tiba mbadala.
Dkt.Mollel ameitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya tafiti za kina kwa wataalamu wa tiba asili kwani NIMR inapaswa kufanya tafiti za kina kuhusu vyanzo vya dawa zinazotumika na kuhakikisha kuwa zinatunzwa vizuri na kuendelea kuzalishwa kwa wingi.
Kwa upande mwingine, Kaimu Mganga Mkuu, Dkt.Ahmad Makuwani, amekiri kuwa dawa zinazozalishwa na wataalamu wa tiba asili zimefanya maendeleo makubwa, huku mataifa mengine kama Angola yakizisajili kama dawa rasmi kwa matumizi ya binadamu.
Kilele cha maadhimisho haya kimewakutanisha waganga wa jadi na wataalamu wa tiba asili, huku kikiwa na lengo la kuboresha huduma za tiba asili na kutetea haki za wanyama katika utendaji wa tiba hizi.