
Jumla ya watahiniwa 5147 waliohitimu katika vyuo mbalimbali, wanatarajiwa kufanya Mtihani wa usajili na leseni unaoratibiwa na Baraza la uuguzi na ukunga Tanzania (TNMC) katika vituo vilivyotengwa kwenye mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Mwanza na Arusha.
Hilo limebainishwa na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa, Mjini Kibaha Mkoani Pwani, alipokutana na wanahabari ili kutoa taarifa kwa umma kuhusu kufanyika kwa mtihani wa usajili na leseni chini ya uratibu wa Baraza la Uuguzi na Ukunga na kwa mujibu wa Sheria ya uuguzi na ukunga ya mwaka 2010.
Usajili amesema mtihani huo utafanyika Ijumaa ya Disemba 20. 2024, ambapo kati ya watahiniwa 5147, wanajumuisha wahitimu ngazi ya Astashahada 86, Stashahada 4498, Shahada ya Uuguzi 537, Shahada ya Ukunga 11 na Shahada ya Uuguzi katika Utaoji dawa za usingizi na ganzi 11.
Aidha, watahiniwa wametakiwa kufika katika vituo vyao kwa wakati na vifaa muhimu ambavyo ni Kalamu Nyeusi (aina ya Obama) au Penseli (HB Orginal) Picha mbili (passport size) Kitambulisho (Indexing card,) Kwa wale wasio kuwa na Indexing kadi wanatakiwa kuja na moja kati ya vitambulisho vifuatavyo; Kitambulisho cha Taifa (NIDA) Kitambulisho cha Mpigakura au Leseni ya udereva na wakiwa nadhifu.
Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania TMNC ni mamlaka ya kisheria inayosimamia wanataaluma na taaluma za uuguzi na ukunga Tanzania, Chini ya Sheria ya Uuguzi na ukunga ya mwaka 2010 na kanuni zake (The Nursing and Midwifery Act 2010) ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini zinakiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.