Madaktari bingwa kutoka Australia kwa ushirikiano na madaktari wa hospitali ya taifa Muhimbili pamoja na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, wameanza zoezi la upasuaji kwa wagonjwa 120 wenye matatizo ya mdomo Sungura kutoka mikoa ya kanda ya ziwa.
Kambi hiyo ya upasuaji wa mdomo Sungura inayofanyikia katika hospitali ya Sekou Toure kwa siku nane kuanzia Aprili 17 hadi Aprili 24, inaongozwa na Dkt. Didier Murcia ambaye ni kiongozi wa timu ya upasuaji kutoka rafiki Surgical Mission.
Zoezi hilo linagharimiwa na serikali ya Tanzania na rafiki Surgical Mission ya Australia kwa ufadhili wa kampuni za uchimbaji wa madini za Acacia na mgodi wa dhahabu wa geita (GGM), ambapo gharama za upasuaji kwa kila mgonjwa ni zaidi ya dola 500.
Baadhi ya wazazi waliofika kwenye kambi hiyo ya upasuaji wa midomo sungura kuwapeleka watoto wao wameipongeza serikali kwa kuboresha na kusogeza karibu huduma za afya.
Kambi hiyo imezinduliwa na mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, ambaye amesema zaidi ya wagonjwa 900 tayari wamefanyiwa upasuaji chini ya programu hiyo inayofanywa na rafiki Surgical Mission la Perth Australia katika kipindi hicho cha miaka minane.