
Waziri wa afya Mhe.Ummy Mwalimu amesema serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 inajenga vituo vya damu salama katika mikoa 12 ili kuboresha huduma ya upatikanaji damu na kuwataka kuendelea kuwaripoti wahudumu wa afya wanaofanya biashara ya damu katika maeneo yao ya kazi ili wachukuliwe hatua
Mhe. Waziri Ummy anasema hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuboresha huduma ya upatikanaji damu salama katika mikoa yote nchini ili kusaidia wenye mahitaji wakiwemo kinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao hutumia asilimia 80 ya damu inayokusanywa nchini.
Aidha waziri Mwalimu amesema licha ya serikali kuwekeza nguvu kubwa katika sekta ya afya lakini bado inahitaji mchango wa wananchi mashirika na wadau ili kufikia malengo ya kuhakikisha utoaji huduma za afya unaboreka nchini kwa ajili ya maendeleo.
Wakati huohuo waziri Ummy amepokea ripoti ya benki ya Exim ambayo imesaidia sekta ya afya kwa kugawa vitanda na magodoro 500 kwenye wodi za wazazi katika hosipitali mbalimbali nchini pamoja na kukusanya chupa 400 za damu kutoka kwa wafanyakazi na wateja wa benki hiyo.