Back to top

Lukuvi amfuta kazi afisa mipango miji kwa kuuza hekari 6000 za ardhi

18 July 2019
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.William Lukuvi amemsimamisha kazi afisa mipango miji wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema, Manase Castory Nkuli ambaye awali alikuwa wilaya ya Lindi kwa kufanya ubadhirifu kufoji nyaraka na kuuza hekari 6000 za ardhi kwenye ufukwe wa bahari ya hindi kinyume na taratibu.

Akizungumza kwenye kikao kazi cha wataalam wa sekta ya ardhi nchini Waziri Lukuvi anasema serikali haiwezi kuvumilia ubadhilifu huo kwani afisa huyo hakufuata taratibu za umilikishaji huku akifoji hati jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Waziri Lukuvi pia amesema wizara yake itafungua kanzi data ya kupokea taarifa zote za matapeli wa ardhi nchi nzima na wananchi wataweza kutoa taarifa juu ya watu hao ili washughulikiwe kutokana na kukithiri kwa matukio ya utapeli na dhuluma kwenye sekta hiyo huku wahanga wakubwa wakiwa ni wantu wanyonge wasio na uwezo.

Kikao kazi hicho pia kimehudhuriwa na wawakilishi kutoka wizara za ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa na menejimenti ya utumishi wa umma ambapo katibu mkuu TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga anasema zipo baadhi ya sheria ardhi zinapashwa kufanyiwa marekebisho ili kuondoa muingiliano wa maamuzi kati ya wizara hizo mbili.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dorothy Mwanyika anabainisha kuwepo changamoto ambazo bado zinaikabili sekta ya ardhi na kutaka watendaji hao kutumia kikao kazi hicho kuzijadili na kutoa maamuzi yatakayowezesha sekta ya ardhi kuwa na nchango mkubwa kwa maendeleo ya wananachi  na taifa.