Back to top

Uwezo wa reli ya TAZARA kusafirisha mizigo washuka

18 December 2018
Share

Meneja wa TAZARA mkoa wa Tanzania Bw.Fard Abdallah amesema uwezo wa reli ya TAZARA kusafirisha mizigo umeshuka kutoka tani milioni tano hadi kufikia tani milioni moja kwa mwaka.

Hayo ameyabainisha mbele ya waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, mhandisi Isack Kamwelwe alipotembelea karakana kuu ya reli ya TAZARA, iliyopo jijini Mbeya na baadaye kufika katika kiwanda cha kuzalisha kokoto na mataluma ya reli hiyo kilichopo kijiji cha Kongolo Mswiswi wilayani Mbarali huku akieleza dhamira ya serikali ya kuboresha reli hiyo.

Waziri Mhe. Kamwelwe amesema serikali imeanza kufanya maboresho makubwa ya miundombinu ya reli ya Tanzania na Zambia, TAZARA, ili  baadhi ya mizigo mikubwa inayoelekea nyanda za juu kusini na nchi jirani ya Zambia isafirishwe kwa njia ya reli kwa lengo la kuzuia uharibifu wa barabara na kuepusha ajali za mara kwa mara za malori ya mizigo mizito na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo.

Wafanyakazi wa reli ya TAZARA wilaya ya Mbeya wamesema mbali na uchakavu wa miundombinu hasa vichwa vya treni, zipo changamoto nyingine nyingi zinazokwamisha ufanisi wa reli ya TAZARA ikiwemo maslahi duni ya watumishi, uhaba wa wafanyakazi na ucheleweshaji wa malipo ya malimbikizo ya fedha za wafanyakazi.