
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amezitaka Taasisi za Dini nchini kuanzisha Idara ya Milki itakayosimamia masuala yote ya ardhi na majengo zinazomilikiwa.
Waziri Silaa ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara katika jengo linalodaiwa kumilikiwa na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) lililopo mtaa wa Chaga Kariakoo ambalo limekuwa likitumiwa na baadhi ya watu kinyume na matumizi.
Kauli hiyo ya Waziri Silaa imekuja baada ya kupata malalamiko mengi ya Taasisi za dini ambazo zimekuwa zikimiliki ardhi na majengo bila kuwa na utaratibu maalumu ya umiliki jambo linaloleta migogoro mingi kati ya taasisi na baadhi ya watu wanaodai ni mali zao.
Awali Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaji Nuhu Mruma alimueleza Waziri Silaa kuwa jengo hilo lililopo kwenye kiwanja namba 117 kitalu 88 linalomilikiwa na BAKWATA limekuwa likitumiwa kinyume na malengo na baadhi ya watu wanaodai kuwa ni wamiliki wakati jengo ilo liliyolewa kama Waqfu.